Wakala wa Misitu Kanda Kusini wameshauriwa kutoa vibali vya upandaji wa Miti kwa wale wote wanaoomba vibali vya uvunaji wa miti ili kutoa uhalali wa kila mmoja kuvuna katika eneo lake.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa februari 14,2020 alipofanya uzinduzi wa zoezi la Upandaji Miti Kimkoa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Tandika iliyopo Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Byakanwa amesema kuwa ametoa ushauri huo kwa wakala wa misitu kwa kuwa wamekuwa wakitoa vibali vya uvunaji wa Miti kwa watu ambao hawana mashamba ya miti wala misitu inayowapa uhalali wa kuvuna mazao hayo.
“Tuainishe maeneo ya kupanda misitu kwenye maeneo yetu, lakini wale wanaotaka vibali vya kuvuna miti ni lazima wawe na mashamba ya kupanda miti, TFS mnakosea sana mnawapa vibali wasio na mashamba.”alisema Byakanwa
Pamoja na Ushauri huo pia Byakanwa amewataka wale wote wanaofanya biashara ya uvunaji wa miti ikiwemo mkaa na mbao kuwa na mashamba ya miti ili biashara wanazozifanya zitoke kwenye mashamba yao.
Aidha amewataka wakala wa misitu kutoa elimu kwa wananchi juu ya kutengeneza miche ya miti ili iwe fursa kwao lakini pia amewataka wananchi kutunza miti iliyopandwa .
Zoezi la uzinduzi wa upandaji wa miti limefanyika kimkoa katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani na jumla ya miti 500 imepandwa katika sehemu za taasisi za umma ikiwemo Shule, Zahanati na Vituo va afya.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.