Pichani wajumbe wa baraza la Madiwani la Manispaa ya Mtwara-Mikindani wakiipitia bajeti hiyo mara baada ya kuwasilishwa
Katika kikao cha baraza la Madiwani la Manispaa ya Mtwara-Mikindani kilichoketi Januari 18, 2020 Kimepitisha na Kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi yenye jumla ya shilingi Bilioni 35,329,320,489 kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Katika bajeti hiyo Manispaa imepanga kukusanya shilingi Bilioni 4,930,000,000 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani na Ruzuku kutoka Serikali Kuu shilingi 710,061,000, Mishahara bilioni 16,980,752,000 na Miradi ya Maendeleo bilioni 12,708,507,489.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa bajeti hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa Kaimu Afisa Mipango wa Manispaa bwana Mensaria Mrema amesema kuwa bajeti hiyo imelenga katika kuboresha maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa.
Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa huduma ya afya ya kadi ya CHF iliyoboreshwa kwa wagonjwa wasiojiweza kabisa hasa wagonjwa akili pamoja na uwezeshaji wa upatikanaji wa hati, urasimishaji na upimaji katika maeneo ambayo yameendelezwa kabla ya kupimwa.
Aidha Katika kuhakikisha vipaumbele hivyo vinatekelezeka pamoja na mikakati mingine iliyojiwekea Manispaa pia imeongeza mikakati ya kuongeza makusanyo ya ndani kwa kuwezesha ujenzi wa yadi ya nchi kavu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari pamoja na kuwezesha ujenzi wa Jimmy /eneo la Mazoezi katika eneo la kupumzikia la Mashujaa.
Kwa Upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindanimhe. Geofrey Mwanichisye amepongeza wataalamu kwa kazi nzuri ya uandaaji wa bajeti lakini pia amewapongeza Madiwani kwa kuridhia na kuipitisha bajeti.
Aidha amesisitiza wataalamu pamoja na Madiwani kushirikiana pamoja kuhakikisha mapato yaliyokisiwa yanakusanywa na kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo.
‘’Sasa hivi nafasi yetu ni kutafuta fedha, kwa sababu kupanga bajeti ni kitu kimoja lakini ili itimie lazima kuwe na rasilimali fedha, tuhakikishe tunapambana kuhakikisha fedha zinapatikana ili Maendeleo ya Manispaa yetu yaweze kutimia” alisema Mwanichisye
Naye Diwani wa Kata ya Likombe Mhe. Mukhsini Komba amesema kuwa kutokana na Maandalizi mazuri ya bajeti hiyo anaamini watalamu na Madiwani wakishirikiana kwenye kukusanya malengo yatafikiwa bila wasiwasi.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.