Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mwalimu Hassan Nyange amesema kuwa, Manispaa hiyo imeendelea kufanya vizuri kwenye usimamizi na matumizi mazuri ya fedha za umma kulikopelekea kupata hati safi (unqualified opinion) kwa mara ya 18 mfululizo kuanzia mwaka wa fedha wa 2006/2007 mpaka 2023/2024.
Mwalimu Nyange ameyasema hayo Leo Juni 20,2025, kwenye mkutano maalumu wa baraza la Madiwani ulioketi katika Ukumbi wa Boma Mkoani Mtwara, kwa ajili ya kujadili taarifa ya Utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,2024.
Amebainisha kuwa, Pamoja na kupata hati safi, Halmashauri ilipokea hoja 15 katika ukaguzi uliofanyika mwaka huo, kati ya hizo hoja 12 zimefanyiwa kazi na kufungwa na hoja 3 zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara COL.Patrick Sawala ametoa pongezi kwa baraza la madiwani na watendaji wa Manispaa kwa kupata hati safi kwa miaka kumi na nane pamoja na usimamizi mzuri wa masuala mbalimbali ikiwemo miradi ya Maendeleo.
“Manispaa hii imekuwa ni miongozi mwa halmashauri inayofanya vizuri kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, afua za lishe, ufaulu wa darasa la saba, kidato cha nne na cha sita, usimamizi wa rasilimali watu na mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, hongereni waheshimiwa Madiwani na watendaji, ninategemea mtakuwa Manispaa ya mfano hapa Tanzania”amesema Col. Sawala.
Aidha ameiagiza Menejimenti kuhakikisha inazifanyia kazi na kuzifunga hoja zilizobaki hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu na amesisitiza kutoweka mazingira ya kutengeneza hoja nyingine kwa kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya matumizi sahihi ya fedha za Umma.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe.Shadida Ndile amemhakikishia Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa hoja zote zilizobaki zitafanyiwa kazi na amemuagiza Mkurugenzi kuhakikisha anazimaliza huku akisisitiza matumizi sahihi ya fedha za Serikali.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.