Bilioni 20 zimetumika kulipa madeni ya Walimu.
Katika kuhakikisha kuwa sekta ya Elimu inaboreshwa na kuimarika Serikali ina mkakati wa kuhakikisha kuwa changamoto za elimu zinashughulikiwa na kumalizwa kabisa ikiwemo utatuzi wa malalamiko ya walimu hasa madeni wanayoidai Serikali.
Mpaka sasa Serikali imelipa madeni ya walimu ambayo siyo ya mshahara kiasi cha Tsh. Bilioni 20 kuanzia mwezi Julai-April 2018 , na kwa upande wa madeni yahusuyo mishahara Wizara ya Utumishi bado wanashughulikia.
Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leornad Akwilapo kwenye sherehe za ufungaji wa Juma la Elimu zilizofanyika kitaifa Wilayani Nanyumbu Mkoani Mtwara kuanzia tarehe 24-28 April 2018. na kuratibiwa na Shirika la Mtandao wa eLIMU tANZANIA (TEN MET)
Aidha Akwilapo amewataka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Kuacha kuisema vibaya Serikali na kutetea walimu kuwa hawafundishi kwa kuwa wanadai stahiki zao.
“CWT acheni udhaifu wa kusingizia walimu hawafundishi kwa sababu ya madeni wanayoidai Serikali kwani madeni yanaendelea kulipwa kupitia mpango wa P4R(Perfomance for result).”alisema Akwilapo.
Kwa upande mwingine Dr. Akwilapo amewataka wanafunzi nchini kusoma masomo ya sayansi ili kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi uliopo kwa sasa. Aliendelea kwa kusema kuwa ingawa Serikali imeajiri walimu 4000 wa sayansi mwaka huu, imeboresha vyuo vya Ualimu 10 na walimu 5900 wamepelekwa vyuoni kupata mafunzo ya masomo ya sayansi ili kupunguza upungufu wa walimu wa sayansi hadi kufikia 2018 bado haijatosha kuondoa tatizo hilo nchini.
Wakati huohuo Akwilapo amewataka wazazi kuwekeza kwenye Elimu na kuiweka elimu kuwa kipaumbele, kuwaachia watoto urithi wa elimu ili kuweza kumuandaa mtoto katika maisha yake ya baadae.
“Tunapaswa kuwekeza katika elimu, hakuna uwekezaji bora kama elimu, mali zote zinaweza kuteketea lakini sio elimu, waachieni watoto urithi wa elimu, elimu haiozi, Elimu ni tunu ambayo mtu hawezi kunyang’anywa.”alisema Akwilapo.
Aidha amewataka walimu kuimarisha usimamizi madhubuti wa ufundishaji na ujifunzaji mashuleni kwani shule za watu binafsi zinafanya vizuri kwa kuwa usimamizi wao ni mzuri na wanafuata kanuni na taratibu za usimamizi wa shule. Pamoja na hayo amewataka pia kuacha tabia ya kuendesha bodaboda badala yake walimu watambue kuwa wao ni ngazi imara ambayo wanafunzi wanapanda ili kufikia malengo yao hivyo wajitume.
Vile vile Katibu Mkuu huyo ametoa agizo kwa wadhibiti ubora wa shule,Viongozi wa elimu wa Wilaya, Viongozi wa siasa kujipanga na kuhakikisha mtoto anapokuwa shuleni anakuwa salama kiafya ikiwemo mtoto huyo kutotumia madawa ya kulevya.
Dr Akwilapo ametoa wito kwa watu wote kuhakikisha Mtoto haachwi nyuma, mtoto anapata elimu, hata mlemavu asiachwe apewe elimu kama kauli mbiu inavyosema 'Uwajibikaji wa pamoja kwa Elimu bora,jumuishi na endelevu'. Aidha amataka Viongozi kuweka mazingira ya shule kuwa rafiki kwa walimu na Wanafunzi ili kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo vyoo, madarasa n.k.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.