DIWANI MTEULE WA KATA YA RELI AAPISHWA TAYARI KWA KUANZA KAZI.
Diwani mteule wa Kata ya Reli Mh.Genfrid Mbunda amekula kiapo cha udiwani baaada ya kushinda uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Reli uliofanyika Novemba 26 na kupata kura 422 ambayo ni sawa na asilimia 50.96
Akizungumza Katika hafla fupi ya kuapishwa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa Mtwara-Mikindani Novemba 30 mwaka huu Naibu meya wa Manispaa Mh.Shadida Ndile amemtaka diwani mteule kuwa muadilifu na kushirikiana na Madiwani wenzake pamoja na watendaji ili aweze kufanya kazi vizuri
Aidha Ndile amesema kuwa kazi nyingi za halmashauri ni za kujitolea hivyo amewaomba Wananchi wa Reli kumpa ushirikiano wa kutosha diwani wao ili waweze kuleta Maendeleo na mabadiliko kwenye Kata ya Reli.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa Mtwara-Mikindani bi Tamko Ally amempongeza diwani mteule kwa ushindi alioupata na kumkaribisha Manispaa kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi wa Reli kwa kuwa wana imani nae na wamempa dhamana hiyo.
Tamko amesema ana imani kuwa kwa kipindi chote cha uongozi wa diwani huyo atawatumikia wananchi wake kwa kufuata sheria, miongoza na kanuzi zote zinazoongoza Manispaa ya Mtwara- Mikindani. Aidha amemkabidhi vitendea kazi vikiwemo kanuni za kudumu za halmashauri, majukumu ya madiwani, Ratiba ya vikao vya mwaka vya halmashauri, mipaka ya kijiografia ya manispaa, kitabu cha maadili ya madiwani, ilani ya Chama Cha Mapinduzi na nakala ya kiapo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya Salumu Mhapi amewashukuru wasimamizi wa uchaguzi kwa kuwa wamejitahidi sana kusimamia haki ndio maana uchaguzi umeisha salama na hakuna vurugu zilizojitokeza.
Akitoa neno la shukrani kwa Wananchi wake Diwani mteule wa Kata hiyo amewaomba ushirikiano wananchi katika utekelezaji wa majukumu yake kwani yeye peke yake hataweza kufanikiwa.
“Kazi zangu zinatokana na nyinyi nategemea uongozi na ushauri ili niweze kufanya kazi vizuri katika Kata ya Reli na kuleta Maendeleo” alisema Mbunda
Uchaguzi mdogo wa Udiwani nchini umefanyika Novemba 26 mwaka huu na kwa Manispaa ya Mtwara Mikindani vyama vitano vya siasa vimeshiriki uchaguzi huo vikiwemo ACT-Wazalendo, CCM, CHADEMA, CUF na NCCR- MAGEUZI.
Katika uchaguzi huo Diwani mteule ambae aligombea kwa tiketi ya Chama Chama Mapinduzi amepata kura 422 sawa na asilimia 50.96, akifuatiwa na CHADEMA kura 356 sawa na asilimia 42.99, ACT- Wazalendo kura 27 sawa na asilimia 3.26, CUF kura 21 sawa na asilimia 2.53 na NCCR Mageuzi kura 2 sawa na asilimia 0.24
Idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura katika Kata ya Reli ni 2320 na idadi ya waliopiga kura ni 842 sawa na asilimia 36.29
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.