Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Sino Tanzania Friendship Mwalimu Riyadh Kadhi amesema kuwa sera ya Elimu bure imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha ufaulu katika Shule za Sekondari hasa za Kata kwa kuwa Shule zinapata fedha kila mwezi zinazowarahisishia katika utendaji wa kazi ikiwemo ufanyaji wa mitihani na ununuzi wa vitendea kazi kama fotokopi Mashine.
Riyadhi amesema hayo Feb 7,2020 alipotembelewa na kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mtwara Mjini ilipofanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa madarasa mawili katika Shule hiyo.
Amesema kuwa Shule ya Sino imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya Mitihani ya Kitaifa ya kidato cha nne mwaka jana imetoa mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza pointi nane akiwa ni mwanafunzi wa tatu kuongoza kiufaulu katika Mkoa wa Mtwara akitanguliwa na wanafunzi wawili waliopata daraja la kwanza pointi saba kutoka Shule ya Sekondari ya Mtwara Ufundi na Abbey.
Aidha Riyadhi ameongeza kuwa wao kama walimu wa Shule ya Sekondari ya Sino wamekusudia kuifanya Shule hiyo kuwa Kituo cha Elimu kwa Kata ya Ufukoni na Mtwara kwa kufaulisha wanafunzi wengi zaidi na kuondoa sifuri ili kuondoa dhana dhaifu na mtazamo finyu wa wananchi kuhusu Shule za Kata.
“Kwa mwaka huu tunao wanafunzi 110 wanaotarajia kufanya Mtihani wa Kidato cha nne malengo ni kuhakikisha Zaidi ya wanafunzi hamsini na tano wataenda kidato cha tano na waliobakia waende katika vyuo vya Maendeleo ,Kilimo na pia tumedhamiria kuondoa sifuri katika Shule yetu” alisema Riyadhi.
Kwa upande wake Mwenyekiti ameipongeza Shule ya Sekondari ya Sino kwa kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa Kidato cha nne ya mwaka jana kwa kutoa mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza kwa pointi nane na kuwataka waongezee bidii ili waweze kufanya vizuri Zaidi.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.