Katika kuelekea kwenye miaka 60 ya Uhuru , Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brig. Jen.Marco Elisha Gaguti amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kuhuisha sekta ya utalii ili kutangaza mali kale zinazopatikana ndani ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
“Tunapoelekea katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wetu, kila mwananchi ana wajibu wa kushirikiana na Serikali ili kukuza sekta ya utalii katika Manispaa yetu” Amesema Gaguti
Gaguti ametoa rai hiyo Desemba 3,2021 katika ufunguzi wa maadhimisho ya sherehe za miaka 60 ya Uhuru yaliofanyika kimkoa katika eneo la Mji Mkongwe uliopo Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Ameendelea kusema kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuipeperusha vema bendera yetu katika sekta ya utalii ndani ya Manispaa yetu hivyo amewataka wadau kujitokeza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha azma hiyo.
Aidha amewashukuru waasisi waliopigania Uhuru wa Tanganyika na kuwataka wananchi wa Manispaa hii kuwaenzi waasisi hao kwa kuendelea kuilinda amani katika maeneo yao.
Naye mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara Mhe. Yusufu Nannila amesema Uhuru huu una maana kubwa sana kwa Taifa katika kuleta maendeleo , hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuulinda na kuudumisha.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Mhe. Abdallah Chikota amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu Mkoani Mtwara hasa katika sekta ya afya na elimu.
Maadhimisho ya siku ya Uhuru Mkoani Mtwara yamefunguliwa Desemba 3,2021 na yataendelea kuadhimishwa hadi desemba 8,2021 yatakapohitimishwa tena Katika Viwanja vya Mji Mkongwe wa Mikindani huku yakichombwezwa na kauli mbiu inayosema “Miaka 60 ya Uhuru, Tanzania Imara, Kazi iendelee”
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.