Ikiwa zimepita siku 25 tangu Uzinduzi wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambapo Manispaa ya Mtwara- Mikindani ilipokea kiasi cha Tsh.440,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 22 vya madarasa kwa shule za Sekiondari, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya amewataka wajumbe wa Kamati za manunuzi katika ujenzi huo kuhakikisha wananunua vifaa vya ujenzi kutoka viwandani ili kupunguza gharama za ujenzi.
Amesema kuwa ununuzi wa bidhaa kutoka viwandani unazingatia ubora na unapunguza gharama zisizo na msingi ambapo fedha hizo zinaweza kuelekezwa katika miradi mingine.
“Ukinunua bidhaa toka viwandani inapunguza gharama na pia unaweza kusevu hela ambayo unaweza kuitumia katika miradi mingine mfano hata ujenzi wa ofisi za walimu” Amesema Kyobya
Mhe. Kyobya ametoa rai hiyo Novemba 4,2021 katika Ziara ya Kamati Kuu ya Mkoa wa Mtwara ilipotembelea kukagua na kupokea taarifa ya utekelezaji wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa kupitia Mpango wa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 katika Manispaa Yetu.
Aidha amewataka wajumbe hao kuzingatia ubora katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi lakini pia kushirikiana katika utendaji wao ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao katika ujenzi huo.
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Bi. Tamko Ally amesema kuwa tayari ofisi yake imeshaanza utekelezaji wa ununuzi wa vifaa vya ujenzi toka viwandani ambapo saruji inayotumika katika ujenzi huo imeagizwa kutoka katika kiwanda cha saruji Dangote.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na amemhakikishia kuwa madarasa hayo yatakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Kamati hiyo imetembelea Ujenzi wa vyumba vya madarasa Sekondari ya Sabasaba,Bandari, Shangani,Chuno,Magomeni ,Mitengo Mangamba na Naliendele pamoja na Shule ya Msingi Mitengo na Kamabarage,
Pia imetembelea Ujenzi wa nyumba ya Mganga Zahanati ya Rwelu na Ujenzi wa Jengo la kujifungulia Zahanati ya Ufukoni pamoja na Upandaji miti iyopo chini ya mradi wa Kaya Maskini TASAF.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.