Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe Evod Mmanda August 16,2018 amezindua Kampeni ya kitaifa ya upimaji wa VVU ijulikanayo kama “FURAHA YANGU” inayolenga kuhamasisha umma wa watanzania hususani wanaume kujitokeza kwenye zoezi la upimaji wa hiyari wa virusi vya UKIMWI na kuanza kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi kwa wale wote watakaogundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Akiongea kwenye uzinduzi huo uliofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa vilivyopo Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mmanda amesema kuwa pamoja na kuhamasisha wananchi wote lakini mkazo zaidi umewekwa kwa wanaume kwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa wanaume wengi hawapendi kupima badala yake wanaweka utegemezi kwa wake zao.
Amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kumuanzishia dawa aliyekutwa na VVU ili aweze kuishi kwa furaha bila ya kuwa na hofu na kuepuka magonjwa nyemelezi kwa sababu kinachoua sio Ukimwi bali ni virusi vinavyopunguza kinga mwilini na kupelekea mgonjwa kushambuliwa na magonjwa nyemelezi na mwili unakuwa jumba bovu hivyo mgonjwa anapotumia dawa anazuia uzalishaji wa virusi.
Aidha Mmanda ametoa rai kwa viongozi wote wa halmashauri kuwa wanatakiwa kuifanya kampeni hiyo kwa miezi sita mfululizo na kuhakikisha kuwa kila mahali penye mkusanyiko wa watu wengi shughuli za upimaji ziwe zinafanyika.
Pamoja na hayo pia ameagiza viongozi wa halmashauri kuhakikisha kuwa vitendanishi na dawa za ARV zinakuwepo za kutosha kwenye vituo vyote vya kutolea huduma na kuwataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la upimaji wa virusi vya Ukimwi na watakaobainika watumie dawa bila kuacha kwa kufuata masharti waliyopewa na wataalamu ili dawa hizo ziweze kufanya kazi mwilini.
"kuna watu wanagundulika na virusi, wanaanzishiwa dawa na madaktari, wanageuka madaktari wanaaza kujipangia mfumo mwingine wa maisha tofauti na ule walioelekezwa na wataalamu, matokeo yake unakuta dawa hazikolei, hazikidhi yale mahitaji yanayotakiwa mwilini kwa hiyo malengo na matarajio ya kufubaza yanakuwa hayajakamilika"alisema Mmanda
Kwa upande wake Mratibu wa kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI Mkoa wa Mtwara Dkt Makarious Moris amesema kuwa Msingi wa kampeni ya FURAHA YANGU ni kutoa huduma za kitabibu ,kitabia na kimfumo. Aidha Kamapeni hiyo ina ushirikishwaji wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla katika harakati za kutokomeza maambukizi ya ukimwi.
Amewataja walengwa wanaoguswa na mradi huo kuwa ni pamoja na watu wote ambao hawajahi kupima virusi vya Ukimwi na wapo katika hatari ya kuambukizwa au kuambukiza, watu wanaoishi na walioathirika na UKIMWI, viongozi wa dini na kiserikali pamoja na watoa huduma katika vituo na jamii. Aidha Kamapeni hii inahusisha afua za kitabibu, kitabia, afua ya mfumo pamoja na huduma ya afya.
Afisa Mradi wa HIV na kifua kikuu kutoka taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation Mkoani Mtwara Dkt Rose Kaaya amesema kuwa mradi wa Kampeni ya FURAHA YANGU unatekelezwa na taasisi hiyo katika mikoa minne ya Tanzania bara ikiwemo Manyara, Tanga, Mtwara na Arusha. Aidha kwa Mkoa wa Mtwara mradi huu unatekelezwa katika halmashauri mbili za Manispaa ya Mtwara-Mikindani pamoja na halmashauri ya Mji Masasi na utafanyika kwa miaka mitatu.
Amesema kuwa Upimaji utafanyika katika ngazi ya jamii ukidhamiria kuzifikia wilaya 8 na Kata 184 zilizopo katika Mikoa hiyo, aidha jumla ya Kaya zisizopungua 281 zilizopo kwenye Kata zinatarajiwa kufikiwa.
Kampeni hii ya kitaifa ya upimaji wa VVU kwa hiari ilizinduliwa rasmi Juni 19,2018 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Khasim Majaliwa kwenye viwanja vya Jamuhuri Mkoani Dodoma. Kauli mbiu ya Kampeni hii ni “FURAHA YANGU PIMA, JITAMBUE, ISHI”. Pamoja na uzinduzi huo pia shughuli mbalimbali za upimaji wa maleria, upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi,upimaji wa shinikizo la damu na sukari,utoaji wa damu salama,utolewaji wa elimu ya uchangiaji wa mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa(CHF iliyoboreshwa) umefanyika.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.