Kutokana na uwepo wa viwanja vingi ambavyo vimemilikishwa kwa muda mrefu ( zaidi ya miaka 20) na kutokuendelezwa kabisa kinyume na masharti ya umiliki na uendelezaji ardhi yaliyoainishwa katika hatimiliki za viwanja husika, Kamati ya MipangoMiji Manispaa ya Mtwara-Mikindani imetembelea Viwanja Saba vilivyopo maeneo ya Mjini katika kata ya Shangani, Chuno na Magomeni na kupendekeza kufutwa kwa miliki za viwanja hivyo ambavyo vimemilikishwa kwa muda mrefu na havijaendelezwa.
Kamati hiyo imejiridhisha na mapendekezo ya ufutaji wa miliki za viwanja husika na hivyo kuelekeza kuwa taratibu zote za kisheria zifuatwe na mapendekezo ya ufutaji au ubatilishaji wa miliki hizo yawasilishwe kwenye ngazi zinazohusika ili
taratibu za ufutaji wa miliki hizo zitakapokamilika, viwanja hivyo viweze kugawiwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji na uwezo wa kuendeleza kwa wakati.
Mkuu Idara ya Mipango Miji Bwana Maiga Rugembe amesema kuwa zoezi la ukaguzi wa viwanja visivyoendelezwa pamoja na kuchukua hatua za kubatilisha au kufuta miliki za viwanja visivyoendelezwa ni endelevu na litaendelea kufanyika kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ardhi sura 113 na Kanuni zake za mwaka 2001
Aidha ametoa Rai Kwa wananchi wote wanaomiliki Viwanja katika maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kutekeleza masharti ya umiliki yaliyoainishwa kwenye nyaraka zao za umiliki (Hatimiliki).
Amekumbusha masharti hayo kuwa ni pamoja na kulipia Kodi ya pango la Ardhi kwa kila mwaka, Kuendeleza viwanja ndani ya kipindi cha miezi 36 tangu walipomilikishwa kwa kupewa kibali cha ujenzi kutoka Halmashauri husika, Kulinda na kutunza alama za mipaka ya kiwanja pamoja na kulinda na kutunza kiwanja au viwanja dhidi ya uvamizi au uharibifu wowote.
Ameendelea kusisitiza kuwa Kushindwa kutekeleza masharti hayo ni kukiuka masharti ya umiliki na hivyo kupelekea kufutiwa umiliki na kiwanja/ viwanja husika.
Aidha amewataka wamiliki wa viwanja kurekebisha kasoro / dosari hizo za umiliki kwa kuzingatia na kutekeleza masharti ya umiliki ili kuepuka kufutiwa haki ya umiliki wa viwanja vyao.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.