Wajumbe wa mabaraza mapya ya Kata Manispaa ya Mtwara-Mikindani wametakiwa Kutenda haki, kutunza siri, kujiepusha na rushwa na vitendo vya dhulma wanaposuluhisha migogoro ili wananchi wayaone mabaraza hayo kuwa ni sehemu ya kukimbilia.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mwalimu Hassan Nyange Leo Januari 15,2025 wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa mabaraza mapya ya Kata tisa za Manispaa yaliyofanyika katika Shule ya Msingi ya Tandika.
Mwalimu Nyange amesema kuwa anatambua umuhimu wa mabaraza katika usuluhishi wa migogoro hivyo ameahidi kuwapa ushirikiano na kukutana nao kila baada ya miezi sita kuona kama yanakwenda vizuri na penye changamoto ili aweze kuzitatua.
Aidha amewaasa Maafisa Watendaji wa Kata wote kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa wajumbe ili kuondoa migogoro ikiwemo ya ardhi ambayo imekuwa kero ndani ya Manispaa.
Kwa upande wake, Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Mtwara Charles Mzava amewasihi wajumbe hao kutolewa Madaraka ya uongozi na kuwataka kutumia busara na hekima katika kusuluhisha migogoro mbalimbali itakayopokelewa katika mabaraza yao.
Nae Mwenyekiti wa baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Mtwara Ndugu. Nadhiru Mbukulike amewahimiza kuwa waaminifu na waadilifu wanapotimiza majukumu yao ili kuepusha kuwa sehemu ya kuzalisha migogoro mipya.
Awali akitoa maelezo kuhusu umuhimu wa uwepo wa mabazara hayo kwenye Kata, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria Manispaa ya Mtwara-Mikindani Allen Ndomba amesema kuwa mabaraza hayo yameundwa ili kufanya usuluhishi baina ya mlalamikaji na mlalamikiwa ili kuleta amani na utulivu katika jamii.
Aidha Ndomba amewasisitiza wajumbe hao kusuluhisha migogoro watakayoipokea pasipo kutanguliza maslahi binafsi na kuzingatia mila na desturi za maeneo husika ili usuluhishi wa migogoro hiyo iweze kufikia mwisho mzuri
Kwa mujibu wa muongozo uliotolewa na TAMISEMI mabaraza ya Kata yana kazi ya kusuluhisha migogoro ya ardhi na ya kijamii iliyopo kwenye Kata na yanafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu tangu kuchaguliwa kwake.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani yapo mabaraza kumi na nane ambapo mabaraza yote yana Mwenyekiti , Katibu na wajumbe ambao wamechaguliwa kwa mujibu wa sheria .
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.