Madiwani Manispaa ya Mtwara Wachagua Naibu Meya
Baraza la Madiwani la halmashauri ya Manispaa Mtwara-Mikindani limefanya uchaguzi wa Naibu Meya pamoja na uundaji wa kamati za kudumu za halmashauri.
Uchaguzi huo unafanyika kila mwaka kwa kuwa ni matakwa ya kisheria ambapo kila ifikapo mwisho wa mwaka baraza linatakiwa kuchagua Naibu Meya pamoja na uundaji wa kamati za kudumu. kanuni za kudumu za halmashauri kifungu namba 7(3)kinatoa ufafanuiz wa mchakato mzima wa uchaguzi huo.
Awali akizungumza kwenye baraza hilo kabla ya uchaguzi kuanza, Msimamizi wa uchaguzi ambae pia ni Mkurugenzi wa Manispaa Mtwara Mikindani bi Beatrice Dominic alisema kuwa amepokea majina 3 ya wagombea wa nafasi ya Naibu meya kutoka katika vyama vya CUF, CHADEMA na CCM.
Aliendelea kusema kuwa wajumbe wanaotakiwa kupiga kura kwenye baraza hilo wako 26 na kuwataka wajumbe wao kuzingatia kanuni na tararibu zote za uchaguzi ikiwemo kutobeba simu unapoenda kupiga kura na kuwasisitiza kuwa kura hizo ni za siri hivyo kila mmoja atachagua mgombea anayemtaka kwa siri.
Hata hivyo kabla ya zoezi la upigaji kura halijaanza wagombea wote walipewa nafasi ya kujieleza,kujinadi pamoja na kuomba kura kwa wajumbe wa baraza. Aidha wapiga kura nao walipata nafasi ya kuuliza maswali kwa wagombea.
Aidha Baada ya kukamilika kwa zoezi la upigaji wa kura msimamizi wa uchaguzi alitangaza matokeo ya uchaguzi huo na kumtangaza Mhe Shadida Ndile kuwa Naibu meya mpya wa Manispaa Mtwara-Mikindani kwa kuwa aliongoza kwa kupata kura nyingi kuliko wagombea wengine.
Mhe Shadida ndile aliongoza kwa kupata kura 14 sawa na asilimia 53, nafasi ya pili imeshikwa na Mhe Selemani I. Mshamu amepata kura 7 sawa na aslimia 26 na nafasi ya tatu imeshikwa na Mh Erick Mkapa kwa kupata 5 kura ambayo ni sawa na asilimaia 19.
Akitoa neno la shukrani Naibu Meya Wa Manispaa mpya Mhe Shadida Ndile alisema kuwa anawashukuru wajumbe wote kwa kumchagua wameonesha wana imani na yeye,aidha ameahidi kufanya kazi kwa kushirikiana na kushikama ili kuongeza kasi ya Maendeleo. Ameahidi pia kufanya kazi na Madiwani wote bila ya kujali itikadi ya chama wala siasa.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe Evod Mmnda amewapongeza Wajumbe wa baraza hilo kwa kuonesha ukomavu wa kisiasa kwani uchaguzi umeanza vizuri na umeisha vizuri bila ya vurugu zozote kama sehemu nyingine zinavyokuwa. Aidha amewataka Madiwani na watendaji kufanya kazi kwa kushirikiana kwa Maendeleo ya wana Mtwara.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri amempongeza Mh Shadida kwa kupata ushindi na kwamba ana imani watafanya kazi pamoja na kwa kushirikiana. Amesisitiza kuwa yeye kama meya wa halmashauri ataendelea kuisimamia na kuitekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwani ndio chama ambacho kipo madarakani.
Kamati za kudumu za halamashauri zilizoundwa ni pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii inayoongozwa na Mhe Hassan Namkami pamoja na Kamati ya Mipango Miji na Mazingira inayoongozwa na Mhe Yakuti T Yakuti.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.