Kuelekea kwenye zoezi la Upimaji, Upangaji na umilikishaji wa ardhi linalotarajia kuanza hivi karibuni katika maeneo ya Mkangala na Mjimwema , Madiwani wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani wamewasisitiza wataalamu wa ardhi kuwa na uwazi uadilifu na uwajibikaji katika kuliendea zoezi hilo.
Waheshimiwa Madiwani wameyasema hayo Disemba 23,2021 katika kikao maalumu cha kutambulisha mradi huo baada ya Manispaa kupokea fedha za mkopo shilingi 1,679,450,000 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kuendesha mradi wa upimaji,upangaji na umilikishaji wa ardhi.
Ili kuepusha watu kulipwa fidia mara mbili mbili Madiwani hao wamewataka wathamini kuwa wakweli kwenye zoezi la uthamini wa mali za watu ili kila mmoja alipwe fidia anayostahili na kuepusha malalamiko yanayoweza kuleta kikwazo katika utekelezaji wa mradi.
Aidha wameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kutupatia fedha hizo na kumtaka Mkurugenzi kutumia mapato yake ya ndani kupima maeneo mengine ambayo hayajapimwa na hayajaguswa na mradi huu ili mji wa Mtwara uweze kupangika vizuri.
Mradi wa Upangaji, Upimaji na Umilikishaji wa ardhi Manispaa ya Mtwara-Mikindani unatarajia kuanza hivi karibuni na utachukua miezi sita hadi kukamilika kwake.
Aidha mradi huu unatarajia kupima viwanja 1200 kwa kupima eneo la ekari 500 katika maeneo ya Mkangala na Mjimwema na viwanja hivyo vitauzwa kwa wananchi kwa bei nafuu.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.