.Idadi ya Vifo imeongezeka na kufikia 13
.Serikali kuhudumia Majeruhi wote
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brig.Jen.Marco Gaguti amewaongoza mamia ya wananchi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani kuaga miili ya marehemu waliopoteza Maisha kwenye ajali iliyohusisha gari lililobeba wanafunzi wa shule ya awali na Msingi ya King David iliyotokea Mtaa wa Mjimwema leo Julai 26,2022 na kusababisha vifo vya watu kumi na tatu na majeruhi kumi na tano.
Akizungumza kwenye zoezi la kuaga miili hiyo lililofanyika kwenye viwanja vya hospitali ya Rufaa ya Ligula Mkuu wa Mkoa amesema kuwa idadi ya vifo imeongezeka kutoka vifo kumi vilivyoripotiwa awali na kutoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu pamoja na majeruhi ambao wanapambania uhai wao.
Amesema kuwa Serikali itatoa ubani wa shilingi laki tatu (300,000) kwa kila familia iliyopoteza ndugu na itasimamia matibabu ya majeruhi wote mpaka pale watakapopata nafuu na kwamba majeruhi watano ambao hali zao haziko vizuri watahamishiwa hospitali ya rufaa ya Ndanda kwa matibabu Zaidi.
Kwa niaba ya Serikali Mhe. Mkuu wa MKoa ametoa pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape Faraja.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Mtwara, Mbunge wa Jimbo la Newala Mhe. George Mkuchika ametoa pole kwa wafiwa na wananchi wa Mtwara kwa msiba mkubwa uliotokea na kuwataka wanamtwara kuamini kuwa hayo ni mapenzi ya Mungu.
Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara Mhe. Yusufu nannila amesema kuwa Chama kimepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba huo na kutoa pole kwa wafiwa na amewasisitiza madereva kuzitumia barabara kwa uangalifu mkubwa ili kuepuka maafa.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.