Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni Mstaafu Mhe. George Huruma Mkuchika (wa kwanza kushoto) akipokea taarifa ya ujenzi wa nyumba ya Mganga Zahanati ya Lwelu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Utumishi na utawala bora Kaptain Mstaafu Mhe George Mkuchika amewapongeza Manispaa Mtwara-Mikindani kwa kuwa halmashauri inayoongoza kufanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya TASAF ukilinganisha na halmashauri zingine zilizopo katika Mkoa huo.
Amesema kuwa kufanya vizuri kwa Manispaa hiyo kumetokana na jitihada zilizofanywa na walengwa wenyewe wa kaya maskini pamoja na usimamizi mzuri unaofanywa na timu ya Wilaya pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Na hivyo kuzitaka halmashauri zingine za Mkoa huo kuiga Manispaa Mtwara-Mikindani.
Pongezi hizo zimetolewa disemba 30, 2017 na Mheshimiwa Waziri kwenye ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara alipokuwa anapokea taarifa utekelezaji wa shughuli za TASAF katika Mkoa wa Mtwara.
Baada ya kupokea taarifa hiyo Waziri Mkuchika amesema kuwa TASAF ni mpango uliobuniwa na Serikali katika kuondoa umaskini katika nchi hivyo ameagiza kuwa watu wote walioingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini kiujanja na hawakuwa na sifa kuondolewa kwenye mpango huo na kuhakikisha wanarudisha fedha zote walizozichukua.
Amesema kuwa lengo la Serikali ni kuifikisha TASAF kwenye vijiji vyote na kwamba hadi sasa asilmia 70 ya vijiji vimefikiwa na asilimia 30 iliyobaki itamaliziwa hivi karibu na kuwataka Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya kusimamia mradi huu kwa kuhakikisha walengwa wanapata fedha kwa wakati, kuhakikisha wale wote waliopatiwa fedha kiujanja na hawakustahili fedha hizo zinarejeshwa na kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatumika kwa wakati ili kosa la kurudisha fedha lisiweze kujirudia.
Aidha Mkuchika amewapongeza Walengwa wa Kijiji cha Rwelu kwa kuibua mradi wa ujenzi wa nyumba ya mganga iliyopelekea kutatua tatizo la kukosa lililokuwa linawakabili la kutopata huduma za afya kwa wakati kwa kuwa mganga alikuwa anaishi mjini (km 15), lakini kwa sasa huduma zote zinapatikana muda wowote kwa kuwa nyumba hiyo imesaidia mganga kuishi kijijini hapo pamoja na mkunga .
Pamoja na hayo Mkuchika amewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto shule na kuwataka kufuatilia Maendeleo ya watoto wao,amewataka kuhakikisha wanawanunulia wanafunzi sare za shule na kuwapatia chakula ili waweze kusoma vizuri na kufanya vizuri katika mitihani yao. Aidha amewataka wazazi na walezi hao kuhudhuria mikutano ya wazazi shuleni.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Gelasius Byakanwa amezitaka halmashauri zilizofanya vizuri kwenye miradi ya TASAF zisibweteke ziendelee kufanya vizuri zaidi na kwamba maagizo yote aliyoyatoa Waziri yatatekelezwa. Amesema kuwa kuhusu walengwa kujiunga na Mfuko wa afya ya Jamii MKoa umeamua kulifanya suala hilo la lazima na ameagiza fedha zitakazotolewa Januari walengwa wote ambao hawajajiunga kwenye CHF fedha zao zitakatwa na watakabidhiwa kadi na kwamba ndani ya miezi miwili asilimia ya walengwa watakaojiunga kwenye CHF itaongezeka kwa zaidi ya asilima 90.
Awali akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Wa kunusuru Kaya Maskini Manispaa ,Mratibu wa Mpango huo bi Sylivia Mwananche amesema kuwa Jumla ya kaya 1328 zilitambuliwa na kunufaika na mpango huo kuanzia March-April 2014. Na hadi sasa jumla ya kaya 1295 zimesalia baada ya zingine kuondolewa kutokana na sababu mbalimbali.
Amesema kuwa Jumla ya Tsh. 876,738,476.00 ya fedha zimehawilishwa kwa walengwa waliopo kwenye mpango kwa mitaa 36. Aidha kwa mwaka 2014/2015 na 2016/2017 Manispaa imetekeleza miradi ya ajira ya muda kwa mitaa 35 ambayo imewezesha walengwa 1287 kujiongezea kipato na fedha jumla ya Tsh. 156,963,400.000 (2014/2015) na Tsh 148,862,900 kwa mwaka(2016/2017) zilihawilishwa.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.