Timu ya ukaguzi wa miradi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Menejiment ya halmashauri wakiwa kwenye picha ya pamoja mbele ya jengo la Mama na Mtoto baada ya kumaliza ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya afya katika Zahanati ya Likombe
Na Jamadi Omari
Manispaa ya Mtwara-Mikindani Hadi kufikia Disemba 31,2017 imefikisha asilimia 93 ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika kituo cha afya likombe na kugharimu kiasi cha fedha shilingi milioni 326,457,759.18 kati ya milioni 500 zilizotolewa na Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo.
Asilimia 7 iliyobaki inatarajia kukamilika baada ya wiki mbili kuanzia Januari 1,2018 na kwamba hadi kukamalika kwa mradi huo Manispaa imekadiria kutumia milioni 400 na kubakiwa na shlingi milioni 100 zitakazotumika katika ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu mingine katika kituo hiko ikiwemo ukarabati wa jengo La OPD , Ujenzi wa choo cha wagonjwa wanaokuja kutibiwa kwenye kituo hicho ambacho kitagharimu Shilingi milioni 15.
Akizungumza kwenye ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo iliyofanyika Januari 1,2018 kati ya Timu ya ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara na Timu ya Menejiment ya halmashauri Mkurugenzi wa Manispaa Bi Beatrice R. Dominic amesema kuwa Ujenzi wa mradi wa miundombinu ya afya unaendelea vizuri na kwa gharama inayoridisha.
Akielezea kuhusu mikakati iliyotumika katika ujenzi huo hadi kupelekea kukisia kubakiwa na fedha zilizotajwa Beatrice amesema kuwa Ofisi yake imetii agizo la Serikali lililotaka mradi huo kujengwa kwa kutumia mafundi wenyeji ambao wametoa gharama za ujenzi zilizo halisi na kazi imekuwa nzuri,na kwamba kila jengo amepewa fundi mmoja na vibarua wake.
Ameongeza kuwa Menejimenti ya halmashauri ilikubaliana vifaa vyote vya ujenzi vinunuliwe viwandani ikiwemo mabati,Gypsum,Tiles,rangi,cable za umeme na vifaa vingine ili kuweza kupunguza gharama na vifaa vichache vilinunuliwa kwenye eneo la Manispaa pamoja na mafundi waliojenga majengo hayo.
Aidha amesema kuwa mradi umefikia hapo kwa kuwa kulikuwa na umakini mkubwa kwenye usimamizi na kwenye kufanya makadirio Lakini pia ushirikiano ulikuwa mkubwa kati ya timu ya halmashauri na Timu ya uendeshaji wa kituo.
Nae Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara Duncan Thebas amepongeza Manispaa kwa kazi nzuri iliyofanyika na kwamba inadhihirisha maamuzi sahihi ya Serikali ya kuikomboa Tanzania kwa kutumia mafundi wenyeji kwenye ujenzi wa miundombinu hiyo. Aidha amepongeza ujenzi wa njia za kupita(walk way) ambayo kwenye maelekezo ya mradi haikuwepo lakini Manispaa imeona umuhimu wa kujenga .
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa DR.Christa Nzali ameishukuru Serikali kwa kuleta fedha hizo kwani kukamilika kwa majengo hayo kutasaidia kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kupunguza vifo vya akina mama na watoto, kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Mkoa.
Wakati huo huo Fundi aliyepewa kazi ya ujenzi wa Wodi ya Mama na Mtoto Athumani Bandiko ameishukuru Serikali kwa kuwapatia kazi ya ujenzi kwani imewapa nafasi ya wao kuonesha uwezo wao kama mafundi wadogo lakini pia imesaidia kutengeneza ajira kwa vijana. AIdha ameiomba Serikali iwaamini na iendelee kuwapa kazi katika majengo mengine.
Manispaa Mtwara-Mikindani Oktoba 13,2017 ilipokea fedha kiasi cha shilingi 500 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika Kituo cha afya Likombe, Miundombinu iliyojengwa ni pamoja na Wodi ya Mama na Mtoto, Maabara, Chumba cha kulaza Maiti, Chumba cha Kufulia nguo, Kichomea taka pamoja na ujenzi wa Nyumba ya Mganga.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.