MANISPAA YAPONGEZWA KWA KUNUNUA GUNIA 200 ZA MAHINDI KWA AJILI YA UJI SHULENI.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Halima Dendego ameupongeza uongozi wa Manispaa kwa kununua gunia 200 za mahindi na kukabidhi kwa walimu wakuu na wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari.kwa ajili ya kupika uji kwa Wanafunzi Shuleni.
Mahindi yaliyonunuliwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa mkoa ambapo aliitaka kila Halmashauri kutenga bajeti ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa chakula cha Wanafunzi.
Akizungumza kwenye zoezi la kukabidhi mahindi hayo lililofanyika Agost 12 kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu Mtwara, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameipongeza Manispaa kutenga bajeti kwa ajili ya kuwapatia chakula wanafunzi shuleni, lakini pia kwa kutekeleza agizo la Serikali.
Hata hivyo Dendego ametaka wazazi na walezi kwa kushirikiana na walimu wao kuona ni namna gani wanaweza kufanya ili watoto waweze kupata angalau mlo mmoja shuleni. Aidha amewataka kutambua kuwa jukumu la kumlisha mtoto shuleni ni la mzazi na walezi.
Awali akitoa taarifa ya zoezi la ununuzi wa mahindi hayo Mkurugenzi wa Manispaa Mtwara Mikindani Bi Beatrice Dominic alisema kuwa gunia 200 za mahindi zilizonunuliwa ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa agizo la serikali na kwamba Manispaa imepanga kununua magunia 500 ya mahindi kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Amesema kuwa Manispaa imetoa mchango lakini wazazi wanatakiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kusaidia Watoto wetu kupata mlo shuleni hivyo wazazi na walezi wawajibike kwa hilo.
Amendelea kusema kuwa mahindi hayo yatagawiwa kwa shule za msingi 31 na sekondari 13 na kwamba ugawaji wa mahindi umezingatia idadi ya wanafunzi shuleni hivyo kuna shule zitapata gunia 2 na zingine zitapata gunia 3. Hata hivyo ameahidi hadi kufikia mwishoni mwa robo ya kwanza 2017/2018 kila shule itakuwa imeshapata gunia 4 za mahindi.
Katika bajeti yake yake ya 2017/2018 Manispaa imetenga kiasi cha shilingi milioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa mahindi ya uji wa Wanafunzi Shuleni na hadi sasa imetumia shilingi milioni 7,600,000 na kununua gunia 200 za mahindi.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.