Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Mwalimu Hassan Nyange, ameendelea kuwasisitiza, kuwatia moyo na kuwapatia maarifa stahiki wanafunzi wa kidato cha nne ili kuwajengea utayari wa kufanya vizuri katika mtihani wa taifa kumaliza kidato cha nne (CSEE).
MD Nyange ameyasema hayo katika ziara yake ya kawaida katika shule ya sekondari Sino -Tanzania Friendship iliyopo kata ya Ufukoni, Manispaa ya Mtwara-Mikindani kwa lengo la kuzungumza na wanafunzi juu ya kuzingatia masomo na umuhimu wa elimu katika maisha.
"Huu ni mwaka wenu wa kufanya maamuzi juu ya maisha yenu, hivyo nawaomba fanyeni maamuzi sahihi yatakayokuwa na faidi kwa maisha yenu ya baadae," alisema.
Aliongeza kuwa wanafunzi hao hawapaswi kuyapa umuhimu mambo yasiyo na tija kama kutazama tamthilia kupita kiasi na kujiingiza katika Mahusiano kwani mambo hayo yatawakosesha dira katika masomo yao.
Aliwasisitiza kwamba hali ngumu ya kimaisha inaweza kuwa changamoto ila haipaswi kuwa kikwazo katika masomo yao, akijitolea mfano yeye binafsi akiwa ametoka katika familia ya kawaida ila mikakati thabiti pekee ndio ilipelekea ufaulu wake.
Alisema kuwa wasiogope kuachana na makundi na marafiki wasio na tabia nzuri na wasio na maadili mema ili wasije kupotoshwa hata kuingia katika mienendo isiyofaa na kupoteza dira kitaaluma.
MD Nyange pia aligusia juu nia yake ya kuandaa kongamano kubwa la wanafunzi wa kidato cha nne kimkoa kwa shule zote za Serikali na binafsi, ambalo litakua na mlengo wa kuwajengea uwezo wa kitaaluma wanafunzi husika.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.