Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Mhe. Shadida Ndile, amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuandaa Mpango Mkakati utakaoweza kutatua tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwani hali hiyo inatia doa taswira ya Manispaa na Taifa kwa ujumla.
Meya Ndile aliyasema hayo leo, tarehe 08 Mei 2025, katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kujadili taarifa za Halmashauri kwa robo ya tatu ya mwaka 2024/2025, uliofanyika katika ukumbi wa Boma uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati thabiti, ikiwa ni pamoja na kuwatafuta wazazi na walezi wa watoto hao ili waweze kuwajibika katika malezi yao.
“Sote tunatambua kwamba hakuna mtoto anayestahili kuitwa mtoto wa mtaani, lakini kuna matatizo ambayo yanahitaji tushirikiane kama wazazi,” alisema Mhe. Ndile.
Aliongeza kwamba kila mtaa una kiongozi anayewajua watoto hao, hivyo ni muhimu kwa kila kiongozi kushiriki katika kuwatambua wazazi wao na kuwakumbusha wajibu wao wa malezi.
Aidha, amekemea tabia inayoongezeka ya watoto kutumika na watu wazima (‘vikongwe’) kuomba maeneo ya biashara, hasa siku ya Ijumaa, wakati ambao wanapaswa kuwa shuleni.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ndile ameitaka jamii kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto na wazee ili kukabiliana na changamoto hii.
Akiahidi kuwa atakuwa mstari wa mbele kuzungumza na wanawake kuhusu malezi, huku akimwomba Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdalah Mwaipaya, kuingilia kati na kudhibiti wimbi la watu wanaotokana maeneo mengine wanaojihusisha na ‘ombaomba’ ndani ya Manispaa.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.