Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mhe. Shadida Ndile leo Februari 27, 2025 amefanya ziara ya ukaguzi wa barabara za ndani (korofi) zilizoharibiwa na Mvua ili kufanyiwa matengenezo kwa haraka.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo Mstahiki Meya amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kupunguza kero ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara kwa wananchi na kutatua changamoto zilizojitokeza wakati kukitafutwa suluhu ya muda mrefu.
Alisema kuwa matengenezo hayo madogo yatafanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani kwa kushirikiana na Wakala ya barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Aidha Mhe. Ndile amebainisha kuwa dhamira ya Serikali ni kupunguza changamoto za wananchi hivyo kama Halmashauri ina wajibu wa kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Katika ziara hiyo Mhe Ndile aliambatana na Mhandisi Ramadhani Mzingwa kutoka TARURA,Diwani WA Viti Maalum Mhe.Zuhura Mikidadi na wataalamu wa Halmashauri hiyo.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu, Ndugu Andy Nyamsangya, kwa niaba ya Mkurugenzi ameahidi kufanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na wataalam hao juu ya suluhu ya changamoto hizo.
Barabara zilizotembelewa ni pamoja na barabara za Kata ya Mtonya, Jangwani, Magomeni, Magengeni na ufukoni.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.