Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Mhe. Shadida Ndile, leo tarehe 05/03/2025 amewaongoza wakazi wa Kata ya Chuno kuanza rasmi wa ujenzi wa uzio kuzunguka shule ya Sekondari Chuno ili kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Wanafunzi shuleni hapo.
Akiongea wakati akitoa neno la shukrani kwa wananchi hao waliojitokeza kwa wingi, Mhe. Ndile alisema jambo hilo ni muhimu kwakua litawaepusha wanafunzi na mazingira hatarishi hivyo kuwafanya wazingatie masomo zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Manispaa Mtwara-Mikindani, Bi. Juliana Manyama alisema hayo yote yanafanyika pia ikiwa ni hamasa kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka Duniani kote.
Naye Mtendaji wa Kata hiyo, Mhe. Khadija Mkongo aliwashukuru wakazi wa kata hiyo waliojitokeza kushiriki zoezi hilo, akiwataka kuendelea na moyo huo na matunda yake watayaona baadae kutokana na matokeo mazuri ya watoto wao.
Makundi mbalimbali yameshiriki ujenzi huo wakiwemo Wazazi wa Wanafunzi, Watendaji na watumishi toka Halmashauri ya Manispaa hiyo, Viongozi wa Chama na Serikali na wengine wengi.
Kaulimbiu ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu ni “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” ambayo imetokana na Kaulimbiu ya Kimataifa ‘’For All Women and Girls, Equality, Rights, Empowerment’’.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.