Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mhe Shadida Ndile amepiga marufuku ya kutowarudisha wanafunzi nyumbani kwa kigezo cha kutomaliza au kutoa michango ya shule badala yake adhabu hiyo wapewe wazazi na walezi kwa sababu wao ndio wenye majukumu ya kuhakikisha michango yote iliyowekwa na shule inalipwa huku akimsisitiza Mkurugenzi kuhakikisha analisimamia swala hilo ili lisijitokeze tena.
“Watoto wetu wanatakiwa wakae shuleni muda wote, inaonekana wanafunzi wanarudishwa shuleni kisa michango, niombe sana katika hili Rais wetu ameendelea kuleta fedha za elimu bure shuleni, yale yanayowahusu wazazi basi wawajibike na sio kuwarudisha watoto nyumbani”amesema Mhe.Shadida Ndile
Mstahiki Meya ametoa agizo hilo leo Mei 26, 2023 kwenye mkutano wa baraza la Madiwani wa kujadili taarifa za halmashauri kwa robo ya tatu uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Chuo Cha Ualimu Kawaida kilichopo Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Pamoja na agizo hilo Mstahiki Meya amewapongeza watendaji na viongozi kwa kuendelea kupambana kuhakikisha suala la ukatili wa kijinsia linapungua na amewasihi wananchi kuendelea kushirikiana kwenye suala la upingaji wa ukatili huo kwenye jamii na kuwafichua wale wanaosababisha maovu hayo ili Serikali iwanyooshe.
Sambamba na hilo amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani kuhakikisha anamalizia ujenzi wa bweni la wanafunzi Sekondari ya Mikindani pamoja na miradi mingine ambayo inaendelea kutekelezwa ndani ya halmashauri imalizike kwa wakati.
Aidha amesema amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiletea Manispaa fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali na kwamba wao kama Madiwani wataendelea kuzisimamia fedha hizo ili miradi iweze kukamilika kwa wakati na katika viwango vilivyokubaliwa.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.