Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mwalimu Hassan Nyange ameahidi kuchangia fedha shilinhi milioni kumi (10,000,000) kwa ajili ya Ujenzi wa bweni la kulala wanafunzi wa kike wakati wa kambi katika Shule ya Sekondari Rahaleo
Akizungumza katika sherehe ya kuhitimu kidato cha nne Oktoba 10,2024 katika viwanja vya Shule hiyo Mwalimu Nyange amesema kuwa lengo la kutoa fedha hizo ni kuunga mkono jitihada za kitaaluma zinazofanywa na shule hiyo kwa matokeo mazuri ya ufaulu wa mitihani ya Taifa ya kidato cha pili na cha nne kwa miaka minne mfululizo.
Nyange amesema kuwa ataandaa utaratibu wa kupita katika Kila Kata kufanya mikutano na wazazi na walezi wa wanafunzi kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuondoa ufaulu wa daraja la nne na sifuri kwa kidato cha nne na kukumbushana suala la malezi kwani malezi bora ndio chanzo Cha ufaulu Kwa mwanafunzi.
Amesema kuwa ifikapo mwaka 2025 atachangia chakula kwa miezi mitatu ya awali kwa shule tano zitakazofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa Taifa kidato cha nne.
Aidha ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wazazi waliohudhuria katika mahafali hayo kuhakikisha wanajiandikisha katika orodha ya majina ya wapiga kura na kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa ifikapo Novemba 27,2024.
Nyange amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kujiandaa na kufanya vizuri katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Julius Mkuwele amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa kutatua changamoto ya kuvuja kwa baadhi ya madarasa na upungufu wa viti na madawati shuleni hapo.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.