Wajumbe wa baraza la Wafanyakazi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani wamempongeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Mwalimu Hassani Nyange kwa kujali maslahi ya watumishi anaowaongoza na kuwalipa stahiki zao Shilingi 444,834,033 katika mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Katibu wa Baraza la Wafanyakazi katika Manispaa hiyo Justine Mkwara amesema kuwa ulipwaji wa stahiki hizo umeleta morali kwa watumishi kufanya kazi kwa kujituma na kuwataka wale ambao hawajalipwa stahiki zao kuwa na uvumilivu kwani malipo haya yanafanyika kwa awamu na kila mmoja atapata haki yake.
Nae Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Mtwara Ndugu Ashrafu Chusi ametoa pongezi kwa Mwalimu Nyange kwa kuwalipa wafanyakazi stahiki zao na kuwa halmashauri pekee ndani ya Mkoa wa Mtwara inayokamilisha vikao vya baraza la wafanyakazi ambapo kupitia vikao hivyo watumishi wanapata nafasi ya kueleza changamoto zao.
“Manispaa ya Mtwara-Mikindani mmepata Mkurugenzi mzuri kuliko halmashauri yoyote ndani ya Mkoa huu, Sisi Vyama vya wafanyakazi tunajua utendaji kazi wa Wakurugenzi wote, Mpeni ushirikiano kama yeye anavyofanya, pendaneni na mumsaidie Mkurugenzi kwenye utendaji wake wa kazi kwa vitendo ili malengo ya halmashauri yatimie na tija ionekane”amesema Chusi
Kwa Upande wake Mkurugenzi Nyange amesema kuwa pamoja na malipo ya stahiki mbalimbali, halmashauri pia imekamilisha malipo ya walimu wa Idara ya Elimu ya Msingi na kwa sasa ataanza kulipa madeni ya walimu wa Sekondari Shilingi 145,000,000 ambapo ameshatoa Shilingi 52,000,000 kama malipo ya awamu ya kwanza na yataanza kulipwa wiki inayofuata huku malipo ya madeni ya watumishi wengine yakifuata.
Aidha amewataka wajumbe wa baraza hilo kuhakikisha wanakusanya maoni, malalamiko, masononeko ya watumishi wanaowawakilisha na kuyafikisha kwenye Menejimenti ili yafanyiwe kazi huku akiwasisitiza kuwapa elimu kuhusu maslahi yao ili kila mmoja atambue haki zake.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.