Baada ya Shule ya Sekondari ya Mtwara Ufundi na Shangani kufanya vizuri kwenye matokeo ya Mtihani wa Taifa wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2024, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mwalimu Hassan Nyange ametoa zawadi ya fedha Shilingi milioni ishirini na tatu laki tano arobaini (23,540,000) na vyeti kwa walimu, wafanyakazi wasio walimu kutoka Shule hizo na baadhi ya wafanyakazi kutoka Idara ya Elimu na Idara zinazosaidiana na Idara hiyo kutoka Ofisi Kuu ya Manispaa ambazo zimekabidhiwa na Mkuu wa Wilaya Mtwara Mhe.Abdallah Mwaipaya.
Mkurugenzi Nyange amesema kuwa ametoa zawadi kwa watumishi hao ikiwa ni sehemu ya kuwapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuwafundisha wanafunzi na kuleta ufaulu mzuri lakini pia ni motisha ambayo itajenga morali ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili matokeo yawe mazuri zaidi kwa miaka inayofuata.
Amesema kuwa lengo la Manispaa ni kuhakikisha kuwa inafuta Daraja sifuri katika matokeo ya mitihani inayofuata na kuongeza kiwango cha ufaulu hivyo amewaagiza walimu wote wa Sekondari kuhakikisha wanamaliza kufundisha ifikapo mwezi wa tano mwaka huu ili wanafunzi wapate muda mwingi wa kufanya mazoezi.
Hata hivyo Mkurugenzi amewataka walimu kuwasaidia wanafunzi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika malezi na makuzi yao ili kuwajenga kiakili ili waweze kusoma kwa utulivu na umakini.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtwara Ufundi Mwalimu Riyadh Kadhi amewashukuru viongozi wa Wilaya na Manispaa kwa kuwatia moyo wakati wote wa maandalizi ya mitihani na kwenye malezi ya Watoto jambo ambalo limepelekea kupata matokeo mazuri kwenye Mitihani hiyo.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.