Mkurugenzi Wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mwalimu Hassan Nyange leo Oktoba 26,2024 amefanya kikao cha wazazi na wanafunzi wanaosoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Chuno ambapo kwa pamoja wamekubaliana kufuta ufaulu wa darala la nne na sifuri kwa kuchanga shilingi 60, 000 kila mwezi itakayowezesha wanafunzi wanaoingia kidato cha nne mwakani kuanza kukaa kambi mwezi Januari ili waweze kujiandaa mapema kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa wa Kumaliza Kidato cha nne.
Mwalimu Nyange amesema kuwa katika fedha hiyo, halmashauri itachangia shilingi elfu thelathini kwa kila mwanafunzi kwa kila mwezi na mzazi atachangia hivyo hivyo kwa mtoto wake.
Ameendelea kusema kuwa katika Uongozi wake hatamani kuona wanafunzi wanafeli hivyo zoezi la kuwaandaa litaanza mapema ambapo ukaaji wa kambi utawasaidia wanafunzi hao kusoma kwa bidii hadi saa nane usiku chini ya uangalizi wa walimu na kufanya mitihani ya upimaji mara kwa mara.
Bwana Selemani Kadeghe mmoja wa wazazi waliohudhuria kikao hicho amewaomba wenzake kuunga mkono jitihada za Mkurugenzi kwa kuhakikisha kila mmoja anachangia fedha hiyo kila mwezi kwa ajili ya watoto wao.
Nae Diwani wa Kata ya Chuno Mhe. Fanikio Chijinga amempongeza Mkurugenzi kwa kuwaunga mkono wananchi wa Kata hiyo huku akiwahimiza wazazi kutimiza walichokubaliana ili kutengeneza kesho iliyo bora kwa watoto wao.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.