Kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mtwara, umetoa msaada wa Vifaa vya kujifungualia (Delivery packs) kwa wanawake wajawazito 24 katika Kituo cha afya Likombe ili kuwasaidia kujifungua salama.
Akizungumza baada ya kugawa vifaa hivyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mhe. Shadida Ndile ametoa rai kwa wanawake wa Manispaa hiyo kufanya maandalizi mapema ikiwemo kuwa na vifaa vya kujifungulia mara wanagundua kuwa ni wajamzito ili kuepusha changamoto zinazoweza kuepukika.
Vilevile amewakumbusha wanawake hao na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanakuwa na bima za Afya ili kuwa na uhakika wa matibabu.
Aidha, amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha Sekta afya hususani katika kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto.
Kwa Upande wake Meneja wa NHIF Mtwara, Dkt. Adolph Kahama, amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko huo inatambua umuhimu wa mwanamke katika ustawi wa jamii na wengi huku wengi wao wakiwa na changamoto za akiba na kumudu gharama za matibabu.
Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dkt. Elizabeth Oming’o ameishukuru NHIF kwa msaada huo na akawasihi wajawazito kuwashirikisha wenza wao na wanafamilia juu ya mahitaji hayo ya msingi ili kurahisisha maandalizi za kujifungua.
Naye Regina Charles akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa msaada huo, amesema kuwa vifaa hivyo vitasaidia kupunguza gharama wakati wa kujifungua.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.