Meneja wa mfuko wa hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa umma (PSSF) Kanda ya Kusini Bwana Sayi Lulyalya amewasisitiza watumishi Manispaa ya Mtwara-Mikindani kuweka mipango ya kustaafu mapema kwa kutunza akiba ya fedha kila mwezi kutoka kwenye mshahara ili kujiwekeza kwenye kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba badala ya kutegemea fedha za mafao ya kustaafu kufanya mambo hayo.
Ameyasema hayo Leo Septemba 13,2022 kwenye kikao cha utoaji wa elimu ya kikokotoo cha mafao ya kustaafu kilichofanyika katika ukumbi wa chuo cha Ualimu kawaida.
Aidha amewataka watumishi hao kujenga utamaduni wa kupitia taarifa zao za michango kila mara ili kuona kama michango hiyo iko sahihi na kuepusha usumbufu pale muda wa kustaafu unakapofika.
Akizungumza kuhusu faida za Kanuni mpya za kikotoo kwa watumishi wa Umma Lulyalya amesema kuwa kanuni hiyo inaongeza kiwango cha mkupuo kutoka asilimia 25 iliyolalamikiwa mwaka 2018 hadi asilimia 33 huku pensheni ya mwezi ikiongezeka kutoka asilimia 50 ya sasa hadi asilimia 67 ya wanachama wa PSPF na LAPF.
Faida nyingine ni pamoja na kanuni hiyo kuweka uwiano na usawa wa mafao baina ya wastaafu wote, itafanya mifuko kuwa imara na endelevu pamoja na kupanda kwa malipo ya mkupuo kwa asilimia 81 ya wanachama na malipo ya pensheni kuongezeka kwa asilimia 19.
Kwa upande wake Bwana. Ephraim Mutkyahwa ameishukuru Serikali kwa kutoa ufafanunuzi wa kikokotoo kwani imeondoa sintofahamu walizokuwa wanazisikia na kwamba ameipongeza Serikali kwa kuweka maslahi mazuri ambayo yakitekelezeka italeta ahueni kwa wastaafu.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.