Baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya Maendeleo iliyotekelezwa kwa viwango vya juu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara mhe Gelasius Gasper Byakanwa hakusita kutoa pongezi kwa Mkurugezi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani bi Beatrice Dominic kwa kuweza kutenga na kutumia fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Pamoja na pongezi hizo amemtaka mkurugenzi kutoifanya jamii ya Manispaa kuwa tegemezi badala yake jamii hiyo ihamasishwe kuweka mikakati ya kuchangia kwenye elimu ikiwemo kuanzisha benki ya matofali yatakayosaidia kwenye ujenzi wa vyumba vya madarsa na nyumba za walimu.
Akizungumza kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofabyika Juni 26,2018 Byakanwa amesema kuwa bado jamii ya Manispaa ipo nyuma kwenye uchangiaji wa shughuli mbalimbali hivyo amemtaka mkurugenzi kutopeleka fedha za ujenzi mahali popote hadi jamii ya sehemu husika iwe imechangia gharama ya ujenzi huo kwa asilimia 20.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amewapongeza wananchi wa mbawala chini kwa kujitoa kwao kwenye ujenzi wa zahanati ya mbawala chini na kuwataka kuendelea kujitolea kwani maendeleo hayana ubaguzi wa aina yeyote
“Niwapongeze kwa kazi kubwa, niwapongeze kwa kutenga ardhi na kusafisha eneo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ni kazi kubwa na mnastahili pongezi, ninawaomba kwa pamoja tushirikiane kuleta maendeleo yetu maana Maendeleo hayana ubaguzi wowote”amesema Byakanwa
Aidha amemtaka Mkurugenzi kuwapa kipaumbele wafanyabiashara wadogo waliopo eneo la mkanaredi kwa sasa kwa kuwapa maeneo ya kufanya biashara ndani ya stendi ya muda ya Chipuputa mara baada ya kukamilika na kuanza uendeshaji wake.
Pamoja na hayo Mkuu huyo wa Mkoa ametoa zawadi ya fedha kwa wanafunzi wa darasa la nne na saba wa shule ya Msingi Singino baada ya kuwauliza maswali na kuyajibu kwa ufasaha. Aidha ameahidi kuwashonea sare wanafunzi watano wa shule hiyo na kuwataka wazazi kuwajibika kuwanunulia sare watoto wao.
Sambamba na zawadi hizo kwa wanafunzi pia ameahidi kuwapatia Ofisi ya Kata ya Jangwani meza na viti kwa ajili ya matumizi ya Ofisi pamoja na bati 50 kwa zahanati ya mbawala chini baada ya kuridhishwa na usimamizi mzuri uliofanyika kwenye majengo hayo..
Awali akiwasilisha miradi ya Maendeleo iliyosomwa mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Manispaa Bi Beatrice Dominic amesema kuwa hadi kufikia Mei mwaka huu Manispaa imefikia asilimia 82 ya ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi Zaidi ya 47 iliyogharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.3.
Amesema kuwa Manispaa inaendelea kutii maagizo mbalimbali yanayotolewa na Serikali ikiwemo kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani katika kuchangia mfuko wa wanawake na vijana na kwamba hadi kufikia May mwaka huu Manispaa imetoa kiasi cha shilingi milioni 433 sawa na asilimia 100. Aidha Manispaa imetoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kidogo cha ushonaji kitakachokusanya wajasiriamali Vijana na wanawake.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara inafanyika ikiwa ni muendelezo wa ziara yake iliyohusisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwenye halmashaurii zote zilizopo Mkoani Mtwara na M anispaa ya Mtwara-Mikindani ni halmashauri yake ya mwisho. Aidha ziara hii kwa Manispaa ya imeanza tarehe 26 Juni na itaishia tarehe 27Juni 2018. Ziara imehusisha ukaguzi wa miradi ya Maendeleo na usikilizaji wa kero mbalimbali za ardhi.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.