Mkuu wa Mkoa Kanali Patrick Sawala ametoa wito Kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kudumisha amani na utulivu wakati wa mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaoendelea.
Ameyasema hayo wakati wa hotuba yake ya kuhitimisha matembezi ya hamasa kuelekea uchaguzi huo pamoja na kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Uwanja wa Nangwandwa Sijaona, Leo 14 Oktoba,2024.
"Mtwara yetu ni nyumbani kwetu usikubali mtu au makundi yoyote kuhamasisha kuleta vurugu, msichezee amani iliyopo, tufanye mchakato huu kwa amani" alisema Kanali Sawala.
Aidha amesisitiza wananchi kuchagua viongozi wastahimilivu, wasikivu, waadilifu, wenye mtazamo chanya na watakaoleta maendeleo na kuendana kasi ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Pia, amewahamasisha vijana wote wenye sifa za kugombea kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi huo.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Abdalah Mwaipaya amesema kwamba ni vema wananchi kufahamu umuhimu wa kuchagua viongozi bora na madhara ya kutochagua viongozi wasio bora.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Mtwara-Mikindani, Mwalimu Hassan Nyange, alitoa rai kwa taasisi, watumishi na wananchi wote Kwa ujumla kutumia siku zilizobakia kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la mpiga kura.
#nyerereday
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.