Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa akikagua mradi wa mfereji mkubwa (km 3.4) wa kuondoa maji ya mvua kutoka skoya, Nabwada,shakur hadi Mtepwezi
Akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Manispaa ya Mtwara-Mikindani kupitia Mradi wa uendelezaji Miji Mkakati(Tanzania strategic Cities Project) na miradi ya TASAF Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe.Gelasius Byakanwa ametoa wiki tatu kwa Kampuni ya simu ya TTCL kuhakikisha inaondoa miundombinu ya nyaya za mawasiliano zilizopo katika maeneo ya utekelezaji wa mradi
Agizo hilo limetolewa leo Novemba 1, 2018 baada ya Mhandisi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Isaac Mpaki kulalamikia ucheleweshaji wa uondoaji wa miundombinu ya Kampuni hiyo katika maeneo ya mradi.
Amesema kuwa TTCL wameshalipwa fedha kiasi cha shilingi milioni 108 za kuhamisha miundombinu tangu septemba mwaka huu lakini hadi kufikia sasa hakuna kilichofanyika.
Aidha Mhe. Mkuu wa Mkoa amezitaka Taasisi zote za Serikali kuwasiliana zinapotaka kutekeleza miradi ili kuepusha usumbufu.
"Ni vema Taasisi zote zinapotaka kutekeleza mradi zikawasiliana kabla mradi haujatekelezwa ili kuondoa gharama ambazo Manispaa imeingia katika kuhamisha Miundombinu "alisema Byakanwa
Pamoja na hayo Mhe Byakanwa amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa mradi kuongeza kasi na kuweka kipaumbele katika ujenzi wa mfereji mkubwa wa kuondoa maji ya mvua unaojengwa kutoka skoya kuelekea Nabwada hadi mtepwezi ili kuondokana na adha ya ujaaji wa maji katika maeneo ikiwemo vifo na upotevu wa Mali.
Vilevile amewataka vijana waliopata ajira kwenye miradi hiyo kuwa waaminifu na kutokuhujumu miradi kwani ni faida ya Wanamtwara.
Byakanwa ameishukuru Serikali ya Tanzania na benki ya Dunia kwa kutenga fedha zilizolenga kuboresha miundombinu ndani ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
" Ninaamini baada ya kukamilika kwa Mradi huu Mtwara itakuwa sehemu nyingine na pengine tunaweza kupata sifa ya kuwa Jiji" alisema Byakanwa
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Kanali Emmanuel Mwaigobeko Amewataka wananchi wa Manispaa kulinda miundombinu inayojengwa na kama kuna mtu MTU yeyote anaoneka anataka kuhujumu mradi basi watoe taarifa mapema katika ofisi yake ili aweze kudhughulikiwa.
Mradi wa uendelezaji Miji Mkakati inatekelezwa na Miji 8 iliyopo Tanzania na kwa Manispaa ya Mtwara-Mikindani ulianza kutelezwa tangu mwaka 2010 hadi sasa kupitia awamu mbalimbali. katika awamu hii ya pili mradi huu unajenga barabara zenye urefu wa km 4.2 Kwa kiwango cha lami, ujenzi wa mfereji mkuu wa kuondoa maji ya mvua wenye km 3.4 ujenzi wa sehemu za kupumzikia 3, ujenzi wa soko la kisasa Chuno na ujenzi wa stendi ya mikindani ikigharimu fedha kiasi Cha Tsh.bilioni 21.7. Aidha wakandarasi wanaojenga mradi huu ni Kampuni ya M/S Jiangxi Geo-Engineering(Group) Corporation kutoka China.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.