Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Evod Mmanda akiagana na Wanafunzi mara baada ya kufunga shughuli za maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika tarehe 8 Machi katika Viwanja vya Mashujaa.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe.Evod Mmanda jana kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa Manispaa Mtwara Mikindani ametangaza vita kwa wale wote watakaobainika kuwapa ujauzito watoto wa kike na kuwakatisha masomo yao.
Amesema kuwa vita hiyo haitaishia kwa wavulana tu hata wanafunzi wa kike watakaobainika kuwa na ujauzito na wazazi au walezi watakaomfumbia macho kijana aliempa ujauzito binti huyo wote watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
“Mabinti mnaosoma na kupata ujauzito hata nyinyi tutakabana labda uwe umebakwa na unaripoti ya Polisi hapo tutashughulika na yule aliyebaka wewe utapata ushauri nasaha, tiba na matunzo mazuri kwa sababu umepata ajali kubwa iliyodhuru mwili wako.
“Na kwa Mzazi ambae binti yake amepata ujauzito badala ya kumbaini kijana mnakaa pande mbili kupatana kama munauziana viwanja kumficha aliyetia ujauzito huku aliyetiwa mimba anaendelea kuteseka na kuwa mzazi asiye na Matunzo tutahangaika na wewe na kwa hili sitatania” alisema Mmanda
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara akikabidhi zawadi kwa mmoja wa wanafunzi wanaofanya vizuri darasani kwneye masomo ya sayansi
Aidha Mmanda ametoa onyo kwa kwa watoto wa kike wanaotumia uzazi wa mpango ili kujikinga na mimba pindi wakiwa shuleni, pia onyo hilo limetolewa na kwa wazazi na manesi wanaowasaidia watoto hao kuwapa uzazi wa mpango.
“Ole wako wewe mzazi, ole wako wewe nesi unaehusika na zoezi kama hili kwa sababu unafikiri unamsaidia mtoto, unapompa uzazi wa mpango maana yake una tambua ana mahusiano sasa unamuambia mwanangu asante jembe hili lima vizuri matokeo yake unamuingiza kwenye kazi mbili shule na mapenzi.
“ninawaambia utazuia mimba lakini si ukimwi na magonjwa ya zinaa kwa sababu ni ishara kuwa ngono zembe inafanyika kwa kutumia uzazi wa mpango maana yake yuko huru, yupo kwenye bahari ya Hindi aogelee kwa nguvu zake hata akifika Msumbiji haya ni matatizo.” Amesema Mmanda
Adha amewataka watoto wa kike kusoma kwa bidii na kutokuwa haraka kwani wanavyoendelea kusonga mbele kielimu ndivyo wanavyojihakikishia kupata Uhakika wa maisha mazuri na kupata mume bora zaidi. Amesema kuwa anatambua wanawake wana jukumu kubwa la kuringa na kujidai kwa majukumu makubwa waliyonayo ya kifamilia na Taifa kwa ujumla.
Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila mwaka Ifikapo tarehe 8 Machi na kwa Manispaa Mtwara-Mikindani maadhimisho haya yaliambatana na ugawaji wa Bima za afya kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, ugawaji wa zawadi kwa watoto wa kike wanaofanya vizuri darasani kwneye masomo ya sayansi, kufanya mazungumzo na watoto wa kike wanaosoma Shule za Sekondari ili kuwatia moyo, Ugawaji wa zawadi kwa wagonjwa waliolazwa Zahanati ya Likombe na kufanya usafi katika zahanati hiyo pamoja na maonesho ya wajasiriamaliali yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa. Aidha kauli mbiu ya mwaka huu inasema“KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA TUIMARISHE USAWA WA JINSIA NA UWEZESHAJI WA WANAWAKE VIJIJINI”.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.