Ikiwa zimebakia siku chache ili Manispaa ya Mtwara-Mikindani iweze kutoa mikopo ya asilimia kumi Shilingi 640,985,000 kwa vikundi 58 vya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu, Mkuu wa Idara ya biashara na Uwekezaji Ndugu Ephreim Kiyeyeu amevihimiza vikundi hivyo kutumia teknolojia ya Habari (mitandao ya kijamii) katika kutangaza biashara zao ili kupata masoko ya uhakika ya kuuza bidhaa zao na kurejesha mkopo kwa wakati.
Aidha amewahimiza kuwa wabunifu kwenye biashara zao ili kuweza kuingia kwenye ushindani wa kibiashara .
Kiyeyeu ameyasema hayo Leo Desemba 30,2024 alipokuwa anatoa elimu ya biashara kwa wajasiriamali waliohudhuria mafunzo ya maandalizi ya kupokeaa fedha za mikopo.
Kiyeyeu ametumia mafunzo hayo pia kuwasisitiza madereva bodaboda wanaotarajia kupata mkopo kuhakikisha wanatii sheria za barabarani na kuhudhuria mafunzo ya udereva na kupata leseni ya udereva ili kuepuka faini mbalimbali zitakazopelekea kushindwa kurejesha mikopo.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Juliana Manyama amewasisitiza wajasiriamali hao kufanya marejesho kwa wakati na kufanya vikao vya mara kwa mara ili kujenga uhai wa kikundi na kushirikisha uongozi pale inapotokea uwepo wa viashiria vya migogoro .
Mafunzo ya wajasiraimali hao yatafanyika kwa siku tatu kuanzia leo Desemba 30,2024 ambapo wataalamu watapita kila Kata kukutana na vikundi vya wajasiriamali vinavyotarajia kupata mkopo wakati halmashauri ikijipanga kutoa mikopo ifikapo Januari 3,2025.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.