Mkuu wa Wialya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya akizungumza na Viongozi wa Kata na Mitaa kuhusu kutoa hamasa ya sensa kwenye maeneo yao
Ikiwa zimesalia takribani siku saba ili zoezi la sensa ya watu na makazi liweze kufanyika hapa nchini, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstany Kyobya ametoa wito kwa viongozi wa kata na mitaa yote iliyopo Manispaa ya Mtwara – Mikindani kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kufanya hamasa kubwa ili wananchi waweze kujitokeza kuhesabiwa.
“Mkafanye hamasa bila woga katika siku chache zilizosalia, hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kama vile makanisani, misikitini, katika vijiwe vya bodaboda na maeneo mengine ambayo sikuweza kuyataja’amesisitiza Mhe. Kyobya.
Amesema kuwa viongozi hao ndio wafanikishaji wakubwa wa zoezi la sensa hivyo wanapaswa kujua kaya zote katika maeneo yao pamoja na kujua changamoto za watu ili kurahisisha zoezi hilo
Mkuu wa Wilaya ametoa wito huo leo Agosti 16,2022 kwenye kikao cha uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya ufundi Mtwara kikihusisha madiwani, watendaji wa kata , watendaji wa mitaa na wenyeviti wa mitaa..
Aidha amewataka Wenyeviti wa mitaa kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa watakaofanya kazi ya kukusanya taarifa za watu na makazi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati.
Kwa upande wake Mratibu wa sensa Mkoa wa Mtwara Bi. Tamali William amewasisitiza viongozi hao kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi ili Mkoa wetu wa Mtwara upate miradi mbalimbali na Manispaa yetu iweze kukua na kupewa hadhi ya kuwa jiji.
Sensa ya watu na makazi hufanyika hapa nchini kila baada ya miaka kumi na mwaka huu sensa ya watu na makazi inatarajia kufanyika ifikapo Agosti 23.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.