Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani COL. Emanuel Mwaigobeko amewataka wafanyabiashara wa Soko la Chuno kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati Serikali ikiendelea kushughulikia mgogoro kati ya wafanyabiashara wa soko la sabasaba na Manispaa ili kupisha taratibu za kimahakama zinazoendelea.
Mkurugenzi ametoa rai hiyo katika kikao chake na wafanyabiashara wa Soko la chuno kilichofanyika mapema leo tarehe 7 Mei 2021 katika viunga vya soko la chuno Mkoani lililopo Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Amesema kuwa , Serikali inaendelea na taratibu stahiki za kimahakama katika kushughulikia mgogoro huo na kesi ipo katika hatua za mwisho, hivyo wafanyabiashara hao wanatakiwa kuwa watulivu na kuendelea na majukumu yao ya kila siku sokoni hapo wakisubiria hatma ya kesi hiyo.
“Naomba nitoe rai ndugu zangu pamoja na ukimya uliopo kesi tayari ipo mahakamani inasikilizwa sio kwamba tumekaa kimya tunapisha taratibu za kimahakama hivyo niwaombe tuwe watulivu wakati taratibu hizo zikifuatwa”alisema Mwaigobeko
Aidha amemtaka mwenyekiti wa soko la chuno Bw. Ally Ndale kuchukua orodha ya vizimba vilivyo wazi (visivyo na biashara) na kutafuta utaratibu maalum wa kuvigawa kwa wafanyabiashara wa soko hilo ambao wamekosa vizimba ili waweze kuendesha biashara zao kwa maslahi yao binafsi na ya Halmashauri kwa ujumla.
“Nikuagize Mwenyekiti wa Soko la Chuno, orodhesha vizimba vilivyo wazi ambavyo havina biashara na uvigawe kwa wafanya biashara ambao hawana vizimba hatuwezi kuona vizimba vipo wazi mwenye chake amestarehe nyumbani wakati mfanyabiashara mwingine anahangaika hana sehemu ya kufanyia biashara’’alisema Mwaigobeko
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mkindani Shadida Ndile amesikitishwa na taratibu zinazoendelea kufanywa na wafanyabiashara wa soko la saba saba ikiwa na pamoja na kuleta vurugu katika maeneo ya soko la Chuno na amewataka waache mara moja na kujikita Zaidi katika biashara zao wakati mahakama ikishughulikia mgogoro huo.
“Nimesikitishwa na taratibu tunazoendelea nazo wana mtwara, misuguano na migogoro tunayoifanya haina tija inarudisha nyuma maendeleo katika Manispaa yetu,mwekezaji hawezi kuja kuwekeza mahali ambapo pana migogoro, tunadumaza maendeleo yetu wenyewe , tujirekebishe na tuendelee kufanya kazi zetu kwa weledi kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla”alisema Shadida
Awali Mwenyekiti wa Soko la Chuno Bw. Ali Ndale amemshukuru Mkrugenzi wa Halmashauri ya Mtwara-Mikindani kwa kukubali wito wa kuzungumza nao na kwa niaba ya wafanyabiashara wa soko la chuno ameomba kupata mrejesho wa kesi kati ya wafanya biashara ya Chuno na Sabasaba.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.