Tukiwa tunaelekea kwenye zoezi la uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Reli unaotarajia kufanyika Novemba 26 2017, Jana tarehe 26 oktoba 2017 Wagombea wa udiwani kutoka katika vyama vitano vya siasa wamerudisha fomu za kugombea kiti hicho.
Zoezi la urejeshaji wa fomu hizo limefanyika katika Ofisi za Kata ya Reli likisimamiwa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Bw. James Tamba akisaidiwa na wasimamizi wengine kutoka Ofisi ya Mkurugenzi pamoja na wasimamizi wa Uchaguzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Uchaguzi.
Wakati zoezi la kukabidhi fomu likiendelea Afisa Uchaguzi wa Manispaa Mtwara-Mikindani Acland Kambili aliwakumbusha wagombea hao kuzingatia Maadili, Kanuni, sheria na taratibu zinazowaongoza kwenye zoezi zima la Kampeni hadi Uchaguzi utakapokamilika
Amewataka wagombea hao kuzingatia sheria hizo na kuwasisitiza kuwa kipindi cha Kampeni wanatakiwa kunadi sera za vyama vyao na kuepuka matumizi mabaya ya lugha ikiwemo matusi, kejeli kwa kufanya hivo kutaepusha aina yoyote ya uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake Jaji Mstaafu ambae pia ni Kamishina wa Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mary Longway amewatakia wagombea kila lenye heri kwenye uchaguzi na kwamba busara itawale na k ana imani maadili wanayajua na wataenda kuyatekeleza.
Nae Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Mtwara-Mjini Beatrice Dominic amewapongeza wagombea hao kwa kuaminiwa na vyama vyao na kupewa dhamana ya kugombea udiwani.Hata hivyo amewasisitiza kusimamia kanuni, sheria,maadili na taratibu zote za uchaguzi zilizowekwa.
Amewasisitiza wagombea pamoja na viongozi wa vyama vya siasa kujenga imani kwa wasimamizi wa uchaguzi kwani bila ya kufanya hivyo kamwe hawataona kuwa uchaguzi ni wa haki. Aidha amewaahidi kuwa wasimamizi wa uchaguzi watapata elimu ya kutosha ili kufanya Uchaguzi uwe wa haki.
“Naomba niwakikishie tutajitahidi tutakavyoweza kuhakikisha kuwa wasimamizi wa kituo kila mmoja atapata mafunzo, elimu ya kutosha kufanya kazi kwa ujuzi na busara ya kutosha, busara ambayo haitaharibu uchaguzi”. alisema Beatrice
Mwajuma Ankoni mgombea wa udiwani kupitia Chama cha ACT-Wazalendo amesema ameridhishwa na mchakato mzima ulivyoanza na imani kuwa kama hali itaendele hivyo basi uchaguzi utakuwa wa amani na kwamba anawaasa wagombea wenzake matokeo yatakapotangazwa wayapokee kwa amani na wale watakaoshindwa wajipange kwa Uchaguzi Ujao.
Vyama vitakavyoshiriki kwenye Uchaguzi huo ni pamoja na chama cha ACT- Wazalendo, Chama Cha Wananchi (CUF), Chama Cha Mapinduzi (CCM) Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha NCCR—Mageuzi. Uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Reli unafanyika baada ya aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo kufariki mwezi Machi mwaka huu.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.