Kampuni ya Utoaji wa mikopo ya Platinum Leo Novemba 10,2022 imekabidhi vifaa tiba vya kujifungulia vyenye thamani ya shilingi milioni sita( 6,000,000) kwa Kituo cha afya cha Likombe ili kusaidia kutatua changamoto wanazokabiliana nazo akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunsta Kyobya ameipongeza Kampuni ya PLATINUM kwa kujitoa kwao na kuisadia jamii kwa kutoa vifaa tiba kwa akina mama wajawazito vyenye thamani ya shilingi milioni sita.
Aidha Mkuu wa Wilaya amewasisitiza watumishi wa Kituo cha afya Likombe kuhakikisha wanavitunza vifaa hivyo ili viweze kufanya kazi kwa muda mrefu, kuwahudumia akina mama wengi zaidi Pamoja na na kupunguza changamoto zilizopo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani COL. Emanuel Mwaigobeko ameishukuru Kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kutoa vifaa tiba ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaenda kusaidia kupunguza mzigo kwa serikali na kutoa wito kwa Makampuni na Taasisi nyingine za biashara kuona umuhimu wa kusaidia jamii kwenye kila faida wanayoipata.
Meneja wa Kampuni ya Platinum Bwana Richard Manyaga amesema kuwa Kampuni yao imetoa vifaa tiba hivyo baada ya kuona kuna changamoto kubwa ambazo akina mama wanakutana nazo wakati wa kujifungua .
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vitanda vya kujifungulia viwili, magodoro mawili, Vifaa vya kujingulia (mama delivery Kit) , mashine ya kupimia mapigo ya mtoto, mashine ya kutakasa vifaa (auto clave) Pamoja na vifaa vingine.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.