Ili kujenga uelewa juu ya matumizi ya gesi asilia na miradi inayotekelezwa hapa nchini, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya ameziagiza shule zote zilizopo Wilaya ya Mtwara kuhakikisha zinanzisha Klabu za mafuta na gesi zitakazosaidia wanafunzi kuwa mabalozi wa kuisemea vizuri gesi .
Pamoja na kuanzishwa kwa klabu za shule Mkuu wa Wilaya pia amesisitiza uwepo wa mazoezi kila mwezi ili kuhamasisha matumizi ya gesi asilia huku akiwaomba Shirika la Mafuta na gesi Tanzania (TPDC) kuendeleza mazoezi hayo mara moja kwenye robo mwaka.
Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo Novemba 12, 2022 kwenye Mbio za TPDC Mini Marathon zilizofanyika katika viwanja vya Nangwanda zikihusisha Shule tano zilizopo Manispaa ya Mtwara-Mikindani, vyuo Pamoja na vilabu vya mazoezi (Jogging Clubs)
Aidha Mkuu wa Wilaya amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kupitia bomba jipya la gesi lenye urefu wa km 35 linalojengwa kutoka Kata ya Nanguruwe hadi Madimba ikikatiza katika vijiji 12 vilivyopo Wilaya ya Mtwara.
Amesema kuwa bomba hilo litakapokamilika uzalishaji wa gesi utaongezeka na kuwataka TPDC kujipanga na kuhakikisha nyumba zote zinaunganishwa gesi na magari yanaanza kutumia gesi ili kupunguza gharama.
Nae Naibu Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mhe. Edward Kapwapwa ameipongeza Kampuni ya TPDC kwa kufanya Mini Marathoni kwa wanafunzi na ameiomba TPDC kuharakisha zoezi la uanzishaji wa matumzi ya gesi kwenye magari ili kupunguza gharama za matumizi ya mafuta.
Awali akizungumza kwenye viwanja hivyo Meneja mawasiliano wa TPDC Maria Mselem amesema kuwa Kampuni yao imeamua kuanzisha Mini marathoni kwa wanafunzi kutoka shule tano za Sekondari zilizopo Manispaa ya Mtwara -Mikindani ili waweze kufahamaiana , kubadilishana uzoefu na kushirikiana kwenye masomo..
Maria amesema amewashukuru walimu kwa kuridhia TPDC kuanzisha Klabu za gesi kwenye shule kumi na saba za Mkoa wa Mtwara na ameomba ushirikiano zaidi ili elimu katika masuala ya gesi na mafuta iendelee kuwepo.
TPDC Mini Marathon Mkoani Mtwara imefanyika kwa lengo la kutoa elimu ya matumizi ya gesi asilia na miradi yake huku ikihusisha Shule za Sekondari tano zilizopo Manispaa ya Mtwara-Mikindani zikiwemo Mangamba Day, Saba Saba , Sino, Bandari na Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara.
Katika mashindano hayo zimetolewa zawadi za fedha taslimu na medani kwa washindi kumi wa mbio hizo.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.