Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara Ndugu Mwinyi Ahmed Mwinyi amewahimiza wananchi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani kuhakikisha wanakunywa kinga tiba za mabusha, matende na minyoo ya tumbo kwa kuwa kinga tiba hizo ni salama na hazina madhara yoyote kwa binadamu.
Amesema kuwa kwa kumeza kinga tiba hizo wananchi wataweza kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kukuza uchumi wa Taifa letu na amewataka viongozi mbalimbali wa kwenye Kata na Mitaa kuhakikisha wanasimamia zoezi hilo kwa kuhakikisha wananchi wao wote wanameza dawa.
Katibu Tawala ameyasema hayo Septemba 4, 2023 alipofanya uzinduzi wa zoezi la Utoaji wa Kinga tiba hizo kwenye Ofisi ya Kata ya Likombe .
Aidha amewapongeza Madiwani kwa kujitoa kumeza dawa hizo kwani italeta hamasa kubwa na kuondoa hofu kwa wananchi ambao wanafikiri kuwa kinga tiba hizo zina madhara kwa binadamu.
Nae Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Mhe. Shadida Ndile ametoa rai kwa watoa huduma waliopata kazi ya kugawa kinga tiba hizo kwa wananchi kuhakikisha wanafanya kazi kwa ukamilifu kwa kupita nyumba hadi nyumba ili Manispaa iondokane na magonjwa hayo hayo kama ilivyo kwa Halmashauri zingine.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya afya Bwana Alex Mkamba amesema kuwa pamoja na wananchi kujitokeza kumeza dawa, amewataka wananchi wenye mabusha kujitokeza ili watambuliwe na waweze kupatiwa huduma.
Diwani wa Kata ya Likombe Saidi Salumu amewataka wananchi wa Likombe kujitokeza kunywa Kinga tiba hizo kwa kuwa Kata yake inaongoza kuwa na watu wenye vimelea vya magonjwa hayo kwa asilimia 6 ukilinganisha na Kata zingine zilizopo Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Zoezi la Utoaji wa Kinga tiba za Mabusha, Matende na Minyoo ya tumbo limezinduliwa leo Septemba 4,2023 na litamalizika Septemba 10,2023.
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.