Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara –Mikindani Bi. Shadida Ndile, amewataka Madiwani wa Manispaa ya Mtwara –Mikindani kutoa elimu kwa wananchi juu ya ukusanyaji na matumizi ya ada ya taka ngumu ili kuleta uelewa wa pamoja.
“Mitambo inayotumika kubebea taka inahitaji ukarabati, lakini pia ada hizo zinatumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Manispaa yetu, tuwape elimu ya kutosha wananchi ili wajue fedha hizo zinatumikaje” Amesema Mhe.Ndile
Mhe.Ndile ametoa agizo hilo Agosti 1, 2021 katika Mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Mtwara Mikindani uliofanyika katika Chuo cha ualimu (TTC).
Ameendelea kusema kuwa sio kwamba wananchi hawana utayari wa kuchangia ada ya taka , baadhi yao hawana uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya fedha hizo, hii inapelekea mwananchi kusita kuchangia ada ya ukusanyaji taka .
Mhe. Ndile ameendelea kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha miundombinu mbalimbali katika Manispaa ya Mtwara Mikindani na amewataka Madiwani kuendelea kuwapa taarifa wananchi juu ya miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.
"Naishukuru sana Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu, Kuna miradi mbalimbali inatekelezwa katika Kata zetu, tutumie vikao vyetu kuwajulisha wananchi maendeleo ya miradi hiyo, sisi wote ni mashahidi juu ya maboresho ya miundombinu, Elimu pamoja na afya ,”Amesema Mhe.Ndile
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.