Watumishi Waaswa Kuacha Kutumia Migomo na Vurugu katika Kudai Haki
Watumishi mkoani Mtwara wametakiwa kufuata sheria na taratibu katika kudai haki badala ya kuwekeza muda na nguvu zao kwenye migomo na vurugu kwani sehemu yoyote yenye vurugu hakuna mafanikio.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mh. Halima Dendego wakati akitoa hutuba yake kwenye sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kwenye viwanja wa mashujaa vilivyopo Mkoani Mtwara.
Dendego amesema kuwa kwa kuwa watumishi wengi wapo kwenye vyama vya Wafanyakazi wawe makini kwenye kuchagua viongozi makini na wenye uelewa mpana na wenye uwezo wa kushawishi ili kuwawakilisha kwenye vikao vya majadiliano na kudai haki.
Aidha Mkuu wa Mkoa amewataka waajiri wote kufuata sheria na kutumia njia ya majadiliano kwenye kufikia makubaliono kwa watumishi wanaowaongoza ,kwani mambo yakuburuzana yameshapitwa na wakati katika dunia hii ya leo.
“Waajiri wote mkoani hakikisheni kuwa sheria za kazi zinafuatwa, waajiriwa wanapata haki zao bila figisu figisu,utulivu unakuwepo mahala pa kazi ili kuunga mkono kauli mbiu ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya HAPA KAZI TU”alisema Dendego
Vile vile Dendego amewataka watumishi walioko kazini na wanaosubiri ajira kujiendeleza kitaaluma ili kushiriki kwenye ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi. Aidha alikumbusha kuwa watu waache ubabaishaji kwani Mkoa umepoteza watumishi 175 katika zoezi lililoendeshwa na Taifa la uhakiki wa vyeti na hivyo kuwataka waajiri kuchukua hatua.
“Ninaagiza Waajiri wa watumishi waliofoji vyeti hakikisheni mnatekeleza agizo la Mh Rais mara moja la kuwafuta katika orodha ya mishahara na stahili zingine”alisema Dendego.
Wakati huo huo Katibu wa TUCTA Mkoa wa Mtwara Bi Masaida Chiwinga aliiomba kuwa Serikali Itilie maanani maoni ya wawakilishi wa Wafanyakazi wakati wa kuandaa viwango vya mishahara kwani Tsh 100,000 ambacho ni kima cha chini kwa mtumishi wa Serikali hakitoshi kukidhi mahitaji.
Alisema kuwa Mkoa wa Mtwara walimu wanaidai Serikali kiasi cha Tsh. 1,809,090,901/= hivyo ameiomba Serikali kuendelea kupunguza madeni haya.
Sherehe za Mei Mosi zinafanyika kila mwaka ifikapi tarehe 1 Mei Dunia nzima wafanyakazi husherehekea siku hiyo. Kwa Tanzania Sherehe hizi zimeazimishwa Kitaifa Mkoani Kilimanjaro zikiwa na kauli mbiu inayosema ‘UCHUMI WA VIWANDA UZINGATIE HAKI, MASLAHI,HESHIMAYA WAFANYAKAZI’
Manispaa Mtwara-Mikindani
Anuani ya Posta: P. o. Box 92,
Simu ya mezani: 023-2333102
Simu ya mkononi:
Barua pepe: md@mtwaramikindanimc.go.tz
Copyright ©2018Mtwara Mikindani Manispaa . All rights reserved.